Showing 1-20 of 111 items.

Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

Hakika Sisi tumeiteremsha Qur"ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia.

Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur"ani hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio jua.

Yusuf alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeota zikinisujudia.

(Baba) akasema: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako, wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shet"ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.

Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa"qub, kama alivyo watimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye hikima.

Kwa yakini katika Yusuf na nduguze ziko ishara kwa wanao uliza.

Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri.

Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa watu wema.

Akasema msemaji kati yao: Msimuuwe Yusuf. Lakini mtumbukizeni ndani ya kisima. Wasafiri watakuja mwokota; kama nyinyi mna sharti ya kufanya jambo.

Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia kheri!

Mpeleke kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze; na bila ya shaka sisi tutamhifadhi.

Akasem: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninaogopa asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.

Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa khasarani.

Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa jambo lao hili, na wala wao hawatambui.

Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.

Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema kweli.

Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza.

Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda.

Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Wala hawakuwa na haja naye.