Showing 1-20 of 83 items.

Ya-Sin (Y.S.).

Kwa Haki ya Qur"ani yenye hikima!

Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,

Juu ya Njia Iliyo Nyooka.

Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika.

Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.

Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.

Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.

Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.

Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.

Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.

Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.

Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.

Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.

Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.

Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.

Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.

Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.

Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.