Showing 1-20 of 135 items.

T"AHA!

Hatukukuteremshia Qur"ani ili upate mashaka.

Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.

Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu zilizo juu.

Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti cha Enzi.

Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi.

Na ukinyanyua sauti kwa kusema...basi hakika Yeye anajua siri na duni kuliko siri.

Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri kabisa.

Na je! Imekufikia hadithi ya Musa?

Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata uongofu kwenye moto.

Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa!

Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako. Kwani upo katika bonde takatifu la T"uwa.

Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa.

Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.

Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya.

Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini na akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki.

Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa?

Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine.

Akasema: Itupe, ewe Musa!

Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio.