Showing 41-52 of 52 items.

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu.

Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo yafanya madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho yao.

Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao tupu.

Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?

Na mkakaa katika maskani zile zile za walio zidhulumu nafsi zao. Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi tukakupigieni mifano mingi.

Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.

Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na ni Mwenye kulipiza.

Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.

Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo;

Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao.

Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo yachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.