Showing 1-20 of 85 items.

H"a, Mim.

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye kujua.

Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna mungu ila Yeye; marejeo ni kwake.

Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu ila walio kufuru; basi kusikughuri wewe kutanga tanga kwao katika nchi.

Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na makundi mengine baada yao. Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki. Kwa hivyo niliwakamata. Basi ilikuwaje adhabu yangu!

Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola wako Mlezi ya kwamba wao ni watu wa Motoni.

Wale wanao beba A"rshi, na wanao izunguka, wanamsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha walio amini kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu.

Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele ulizo waahidi. Na uwape haya pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa.

Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa.

Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya kutoka?

Hayo ni hivyo kwa sababu mlikuwa akiombwa Mwenyezi Mungu peke yake mnakataa. Na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu.

Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na anakuteremshieni kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye rejea.

Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, na wangachukia makafiri.

Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A"rshi. Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa Siku ya Mkutano.

Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana chochote chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu Mmoja Mtenda nguvu.

Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo chuma. Hapana dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa.

(Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua.

Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia Mwenye kuona.