Showing 1-20 of 89 items.

H"a Mim

Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.

Hakika Sisi tumeifanya Qur"ani kwa Kiarabu ili mfahamu.

Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima.

Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri?

Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!

Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.

Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.

Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,

Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka.

Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.

Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.

Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.

Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.

Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.

Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?

Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.

Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...?

Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa!

Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!