Showing 1-20 of 93 items.

T"aa Siin. (T".S.), Hizi ni Aya za Qur"ani na Kitabu kinacho bainisha;

Uwongofu na bishara kwa Waumini,

Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo.

Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo.

Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio watapata khasara zaidi.

Na hakika wewe unafundishwa Qur"ani inayo tokana kwake Mwenye hikima Mwenye kujua.

(Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate kuota moto.

Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu Mitume.

Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu waovu.

Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri.

Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!

Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini.

Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri.

Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.

Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua.

Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?