Showing 1-20 of 128 items.

Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiihimize. Ametakasika na Ametukuka na wanayo mshirikisha nayo.

Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake ili nyinyi muonye kwamba hapana mungu ila Mimi, basi nicheni Mimi.

Ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Ametukuka na wanayo shirikisha.

Amemuumba mtu kwa tone la manii. Naye mara amekuwa mshindani dhaahiri.

Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala.

Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na mnapo wapeleka malishoni asubuhi.

Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo weza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu.

Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na ataumba msivyo vijua.

Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo njia za upotovu. Na angeli penda angeli kuongoeni nyote.

Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.

Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.

Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili.

Na hivi alivyo vieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa watu wanao waidhika.

Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.

Na kaweka katika ardhi milima ili ardhi isiyumbe yumbe nanyi. Na mito, na njia ili mpate kuongoka.

Na alama nyengine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.

Ati anaye umba ni kama asiye umba? Basi hebu, hamkumbuki?

Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.

Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.

Na wale wanao waomba wasio kuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.