Showing 1-20 of 118 items.

HAKIKA wamefanikiwa Waumini,

Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,

Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,

Na ambao wanatoa Zaka,

Na ambao wanazilinda tupu zao,

Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.

Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.

Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,

Na ambao Sala zao wanazihifadhi -

Hao ndio warithi,

Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.

Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.

Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti.

Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.

Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.

Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.

Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe.

Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa.

Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;

Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao.