Showing 1-20 of 110 items.

Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo.

Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.

Wakae humo milele.

Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana.

Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu.

Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya!

Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi.

Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame.

Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?

Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo letu.

Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.

Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa.

Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.

Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.

Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu?

Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.

Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi.

Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.

Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.

Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa!