Showing 1-20 of 37 items.

H"a Mim

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini.

Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.

Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili.

Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake?

Ole wake kila mzushi mwenye dhambi!

Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia yale yale aliyo katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu chungu!

Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha. Watu hao ndio watakao kuwa na adhabu ya kufedhehesha.

Na nyuma yao ipo Jahannamu. Na walio yachuma hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu. Na watapata adhabu kubwa.

Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za Mola wao Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu.

Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.

Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.

Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi.

Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu wote.

Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana.

Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.

Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao.

Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha.