Showing 1-20 of 200 items.

Alif Laam Miim.

Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai, Msimamizi wa yote milele.

Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili

Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani (Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.

Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake, duniani wala mbinguni.

Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili.

(Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji.

Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa Siku isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.

Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni-

- Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa kabla yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi yao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na mtakusanywa, mtiwe kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa.

Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi mawili yalipo pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye macho.

Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema.

Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamngu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake walio takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake,

Ambao husema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumeamini, basi tufutie madhambi yetu, na tuepushe na adhabu ya Moto,

Wanao subiri, wanao sema kweli, na wat"iifu, na wanao toa sadaka, na wanao omba maghafira kabla ya alfajiri.

Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio pewa Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.