Showing 1-20 of 78 items.

Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu.

Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.

Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet"ani aliye asi.

Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.

Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri.

Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.

Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua.

(Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.

Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.

Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali!

Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.

Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake itaondoa hayo yaliyo mkasirisha?

Na namna hivi tumeiteremsha (Qur"ani) kuwa ni Aya zilizo wazi, na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.

Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.

Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.

Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka.

Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao pia.