Showing 1-20 of 286 items.

Alif Lam Mim.

Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu,

Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa.

Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.

Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.

Hakika wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawaamini.

Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao, na juu ya macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu kubwa.

Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.

Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.

Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.

Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.

Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu. Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui tu.

Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao na mashet"ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu.

Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha katika upotofu wao wakitangatanga ovyo.

Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini biashara yao haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka.

Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha katika giza, hawaoni.

Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.

Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.

Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza huenda, na unapo wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.