Showing 1-20 of 75 items.

Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mt"iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.

Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.

Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku.

Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira, na riziki bora, kwa Mola wao Mlezi.

Kama Mola wako Mlezi alivyo kutoa nyumbani kwako kwa Haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.

Wanajadiliana nawe kwa jambo la Haki baada ya kwisha bainika, kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti nao wanaona.

Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.

Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangachukia wakosefu.

Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana mfululizo.

Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.

Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shet"ani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.

Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto.

Enyi Mlio amini! Mkikutana na walio kufuru vitani msiwageuzie mgongo.

Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.

Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa, walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Msikizi na Mjuzi.

Ndio hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya makafiri.

Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kujieni. Na mkiacha itakuwa ndio kheri kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea. Na jeshi lenu halitakufaeni kitu, japo likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini.

Enyi mlio amini! Mt"iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye, nanyi mnasikia.