Showing 1-20 of 165 items.

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi.

Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnatia shaka.

Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma.

Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa wenye kuipa nyongo.

Wameikanusha Haki ilipo wajia. Basi zitawajia khabari za yale waliyo kuwa wakiyakejeli.

Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi kingine.

Na lau tungeli kuteremshia kitabu cha karatasi, wakakigusa kwa mikono yao, wangeli sema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uchawi dhaahiri.

Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha Malaika, basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli pewa muhula.

Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli mfanya kama binaadamu, na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao.

Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia kejeli.

Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.

Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini.

Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.

Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.

Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi.

Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu.

Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari zote.

Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur"ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha.

Wale Tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao. Wale walio zikhasiri nafsi zao hawaamini.