Showing 1-20 of 73 items.

Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat"ii makafiri na wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.

Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia.

Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni.

Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu,

Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu.

Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.

Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali.

Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.

Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.

Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu.

Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.

Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.

Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat"ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu.